Wednesday, November 2, 2011

MNATAKA MUNGU ASHUKE ILI AJE KULINDA MALI ASILI ZETU?

Jukumu la kulinda Mali asili za nchi ni la kila mmoja wetu. Kila Mtanzania ana jukumu la kuhakikisha kwamba mali asili za nchi zinalindwa na kusimamiwa vizuri ili hata vizazi vijavyo viweze kunufaika na mali asili zilizopo nchini. Mbali na jukumu la ulinzi wa mali asili kuwa ni la kila Mtanzania, kuna watu wengine ambao kimsingi wamepewa dhamana ya usimamizi na ulinzi wa mali asili hizi, ambao ni pamoja na watumishi wa idara ya misitu au maafisa misitu, maafisa wanyamapori na maafisa uvuvi.

Lakini jambo la kusikitisha watu hawa wenye dhamana ya usimamizi na ulinzi wa mali asili, ndiyo wanao husika kwa namna moja au nyingine katika uharibifu na upotevu wa mali asili za nchi. Watumishi hawa ama wanapokea rushwa ili kuruhusu watu wafanye uharibifu au ni wazembe katika suala zima la ufuatiliaji ili kuhakikisha mali asili za nchi zinasimamiwa vizuri na kulindwa. Swali langu kwa watumishi hawa ni je, ‘Mnataka Mungu ashuke ili aje kulinda Mali Asili zetu’? Kwasababu wenye dhamana kubwa ya kufanya hivyo wanaonekana kutowajibika ipasavyo au kushindwa kabisa
Tukirejea katika ripoti ya tume ya jaji Joseph Sinde Warioba pamoja na wajumbe wengine kuhusu tatizo la rushwa iliyo tolewa na gazeti la Mwananchi siku ya jumatano juni kumi na tano (15) katika ukurasa wa nne (4), ripoti hii imeonesha kwamba katika sekta ya mali asili na utalii, watumishi wa idara ya Misitu hupokea rushwa na kutoa vibali kwa watu vya kukata miti zaidi ya ile iliyoidhinishwa.

Vilevile watumishi hawa huwaachia watu wanaokamatwa kwa tendo hili ovu wakiwa na mbao au magogo yaliyokatwa bila kibali. Hivi nani asiyejua umuhimu wa misitu na nani asiyejua madhara ya kuharibu misitu? Kwa faida ya wasiojua umuhimu wake ni kwamba husaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta mvua ambayo kwayo huleta faida katika shughili za kilimo, vilievile husaidia katika utunzaji wa ardhi kwa kuzuia mmomonyoko wa udongo, na kinyume chake.

Katika suala hili la uvunwaji wa misitu bila kibali ninao mfano halisi wa msitu wa Pugu ambao upo wilaya ya Ilala nje kidogo ya Mkoa wa Dar es Salaam. Katika msitu huu kuna uvunaji holela wa miti unaoendelea hali inayohatarisha kupotea kwa msitu huo kama jitihada za makusudi hazitafanyika ili kuokoa msitu huo. Imefikia hatua watu wanadiriki hata kujenga nyumba ndani ya msitu huo na kuweka makazi yao, pia wapo wanao choma mkaa ndani ya hifadhi ya msitu. Hivi je, mimi na wewe hatuyaoni haya? Watumishi wenye dhamana ya usimamizi na uhifadhi wa misitu hawayaoni haya? Kama jibu ni ndiyo, wanachukua hatua gani ili kuweza kunusuru jambo hili? Maana wanaonekana kanakwamba wamelala usingizi kabisa.

Hebu tuige mfano wa Meatu ambapo katika miaka ya 1980 ilikuwa moja kati ya wilaya za Mkoa wa Shinyanga zilizo karibia kugeuka jangwa baada ya wananchi wake kufyeka karibu misitu yote kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.Lakini hivi sasa wilaya ya Meatu imepiga hatua kubwa katika utunzaji wa miti na mazingira kwa ujumla ambapo karibu kila sehemu ya wilaya hiyo imejaa miti iliyopandwa na wanachi. Mwaka jana pekee ilipandwa miti milioni 14.9, mafanikio haya yametokana na elimu iliyotolewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji misitu.

Ripoti hiyo imeendelea kuonesha kwamba katika sekta hii, mbali na rushwa iliyopo kwa watumishi wa idara ya Misitu, kuna rushwa kubwa hufanyika kwa Maafisa wanyamapori ambao hupokea rushwa na kuruhusu majangili kufanya uwindaji wa wanyama bila kuwa na kibali maalum. Hili ni jambo hatari na linasikitisha kwani uwindaji huu haramu utasababisha kupungua kwa wanyama kwenye mbuga zetu ambao ni kivutio kikubwa kwa watalii, hivyo kutaathiri sekta ya utalii ambayo licha ya kuwa na changamoto kama hizi huchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa na kuinua uchumi wa nchi. Ikumbukwe kwamba wanyama pia wanahaki ya kuishi kama ilivyo kwa viumbe wengine hivyo uwindwaji unaofanywa dhidi yao unakiuka haki zao. Katika miaka ya nyuma kulikuwa na uwindaji mkubwa wa mnyama Panda ilifikia hatua ya kutaka kupotea kwa spishi hiyo duniani lakini hali hiyo iliweza kudhibitiwa. Hivyo mimi na wewe pamoja na wenye dhamana ya usimamizi wa wanyamapori tunapaswa kufanya jitihada za makusudi ili kuweza kuidhibiti hali hii kwani inawezekana.

Tukiendelea kusalia katika ripoti hii, kwa upande wa uvuvi, rushwa imetawala kupindukia ambapo inatolewa na wavuvi wanaokamatwa kwa tuhuma za kuvua kwa kutumia njia haramu ikiwa ni pamoja na nyavu zisizo stahili (kokoro) na utumiaji wa baruti. Hivi maofisa uvuvi hawafahamu uwepo wa jambo hili au linafahamika lakini linafumbiwa macho?. Ni wazi kwamba njia hizi haramu katika uvuvi huchangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa samaki katika bahari, mito na maziwa yetu kwani kokoro kutokana na udogo wa matundu husababisha hata samaki wachanga kuvuliwa na kutupwa tu wakati wangeweza kuzaliana kwawingi hapo baadaye kama wangeachwa hivyo kuongezeka kwa wingi wa samaki. Utumiaji wa baruti katika uvuvi pia husababisha samaki wengi wadogo kufa mbali na wale wakubwa ambao ndiyo haswa huhitajika.

Hali hii ikiendelea kufumbiwa macho na kupuuzwa, ni wazi kwamba mali asili za nchi zitapungua kwa kiasi kikubwa, hivyo mimi na wewe tunatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha tunalinda mali asili zetu hata kwakutoa taarifa kwenye vyombo husika ili viweze kuchukua hatua stahiki pindi kunapotokea uharibifu katika mali asili za nchi ili kizazi cha sasa na cha baadaye kiweze kunufaika na mali asili zilizopo nchini.
Imeandaliwa na;
Hoffman Hans Sanga-YET – 2011

1 comment:

  1. Hongera Mwandishi. Mungu ametupa akili na utashi yatosha.Tukiamua na Tukataka kutunza mazingira kama Meatu na Hata zaidi yao inawezekana.

    ReplyDelete