Friday, September 18, 2009

MIKUMI IPO HATARINI

Tarafa ya mikumi inapoteza utajiri asilia ambapo binadamu amekuwa ni chanzo kikubwa cha kupelekea kupotea kwa utajiri huo. Katika maeneo mbalimbali ndani ya Tarafa ya mikumi kumebakiwa na nyasi kavu zisizo na uhai pamoja na vumbi ambavyo ni viashiria tosha vya maisha duni baadae.

Hivi sasa hali inatisha ukiangalia maeneo mbalimbali kuzunguka Tarafa hiyo. Katika maeneo hayo kumebakiwa nyasi kavu, maeneo ambayo yamechomwa moto pia miti michache inayoweza kuhesabika hata ukiwa umbali wa mita mia tatu (m.300) toka katika kila eneo la ekari ishirini. Shughuli mbalimbali zinazofanywa na binadamu imekuwa ni chanzo kikubwa cha kupoteza uoto huo. Hayo yalizungumzwa katika mkutano ulioendeshwa tarehe 12.09.2009 na asasi isiyo ya kiserikari ijulikanayo kama Greenbelt Schools Trust Fund (TSGF) kwa kudhaminiwa na WWF katika kata ya Mikumi.

Watu wamekuwa wakifanya shughuli zenye madhara katika mazingira ilikujipatia mahitaji yao ya kila siku. Shughuli hizo ni kama vile utengenezaji wa mkaa, ufugaji holela pamoja na kilimo cha kuhamahama. Hii inaonesha kwamba wenyeji hao hufanya shughuli ambayo itawaletea matunda haraka pasipo kufikiri hasara zinazojitokeza. Mjumbe mmoja wa kamati ya mazingira kutoka WWF Ndugu Angelus Runji amesema “Uwajibikaji mdogo wa wanajamii katika kuhifadhi mazingira ndio chanzo cha madhara mbalimbali kama vile umomonyoko wa udongo na ukame. Vilevile mwenekiti cha Mikumi Ndugu Idd Liko amesema” baadhi ya watu hujihusisha na uchimbaji wa udongo ilikutengeneza tofari, Pia hukata kuni kwajiri ya kuchomea tofari hizo”. Hali hii imedhihilika katika bonde la mto Ruhembe ambapo imepelekea udongo kupoteza rutuba.

Shughuli hizo zimepelekea kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa misitu katika eneo la Mikumi na hatimae kuwepo kwa udongo usiofaa kwa kilimo pamoja na uhaba wa maji. Hali hii imeshuhudiwa na Katibu Mkuu wa Asasi moja isio ya kiserikali ijulikanayo kama Greenbelt Schools Trust Fund (GSTF) (Ndugu John Mengele) inayojishughulisha na mazingira amesema “Pia sababu nyingine inayopelekea uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji ni kilimo holela cha umwagiliaji maji kinachoenda sambamba na ukataji wa miti kandokando ya mto Ruhembe”. Ameendelea kusema kwamba hapo awali mto huu ulikuwa ukijulikana kama Bustani ya asili ambapo ndizi zilijiotea zenyewe kando kando ya mto lakini hivi sasa eneo limekuwa kame.

Huu ni wakati muafaka kwa wanakijiji katika Tarafa ya Mikumi kuchukua hatua madhubuti kuzuia madhara ya uharibifu wa mazingira yanayojitokeza. Hatua hizo ni kama kupanda miti ya matunda, mbao na nguzo. Jitahada hizi zitapelekea kuinua kipato cha wanajamii kwa kuuza matunda, mbao pamoja na nguzo. Pia kutatua tatizo la uhaba wa maji.

Greenbelt Schools Trust Fund (GSTF), imeanzisha mradi wa upandaji miti hasa miti ya matunda kama vile miembe. Asasi hii imelenga kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2012, kila familia imiliki miti hamsini (50) ya aina tofauti.hatua za mwanzo za kutekeleza mradi huo zimeonekana katika mkutano huo ambapo wanakamati waliridhia mradi huo na kupewa mbegu pamoja na miche ya miti wakapande. Jitihada hizi ziliungwa mkono na katibu tarafa wa Mikumi Ndugu Benjamin Mang’ara

Amesema “hiki kilichotokea leo sijawahi kukiona tangu nishike wadhifa huu katika tarafa hii, nidhahili kwamba jitihada hizi zitaboresha maisha ya watu na shughuli zao katika katika ngazi ya kata hata tarafa yetu ya Mikumi. Serikari pia imeona haja ya kuanzisha mpango wa muda mrefu wa upandaji miti ambapo kila familia inapaswa kupanda miti Kumi (10).” ameendelea kusema kwamba jamii ibadili tabia ili kuwepo matumizi endelevu ya rasilimali zetu na hatimaye kupunguza umasikini uliopo.

Hii ni dhahili kwamba hakuna kinachoweza/kitakachoweza kufanyika endapo jamii zetu hazitazingatia matumizi endelevu ya rasilimali tulizonazo.

Angelus Runji
runjifred@yahoo.com

No comments:

Post a Comment