Thursday, September 1, 2011

WANAMAZINGIRA TUJIFUNZE NINI KUTOKA WIZARA YA MALI ASILI NA UTALII?

Hivi karibuni kuliibuka sakata la kutoroshwa kwa wanyama hai nchini kwa kutumia ndege ya jeshi la Qatar uliofanyika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro( KIA).Kwa habari zilizosikika miongoni mwa vyombo vya habari wanyama hai waliotoroshwa kwa njama ni zaidi ya 120 na thamani yao ni takriban sh. Milioni 6.9 ambao ni ndege hai na jumla ya fedha za wanyama wote hai hao ikiwa ni shilingi 170,570,500.

Jambo la kushangaza na kusikitisha ni kwamba wizara hii wanaeleza kwamba haijulikani wanyama wale baada ya kupakiwa pale KIA walipelekwa wapi na kama bado wako hai.Kwa kweli sisi wanamazingira pamoja na umma wa watanzania tumesikitishwa sana jinsi serikali inavyopata kigugumizi katika kushughulikia suala hili hasa katika kuhakikisha kuwa rasilimali hiyo muhimu na adimu iliyoibiwa inarudishwa nchini. Ni jambo la kufedhehesha kuona kwamba tangu utoroshwaji wa wanyama hao ufanyike Novemba 24, 2010 hadi leo bado serikali ilikuwa haijui wanyama hao wako wapi hali inyotia mashaka.

Yapo maswali mengi ya kujiuliza kuhusu suala hili la utoroshwaji wa wanyama hao .Katika wanyama 116 waliotoroshwa wenye thamani ya 163,732,500 ni pamoja na twiga wanne kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa bungeni tarehe 18/08 2011. Swali la kujiuliza kwa nini sheria ya wanyama pori inayozuia raia wa kigeni kupewa leseni ya kukamata wanyama wakiwemo twiga ambao ni nembo ya taifa haikuzingatiwa? Hii ni dalili kubwa ya uzembe na kupotoshana.

Haiwezekani wanyamapori hao wakiwemo twiga, wanyama wakubwa kabisa waibiwe wasafirishwe kutoka mbugani hadi uwanja wa ndege wa KIA, wapakiwe kwenye ndege ya Qatar na hatimaye watoroshwe halafu viongozi wakuu wa wizara ya mali asili na utalii na idara zake wasijue. Hii ni aibu kwa taifa ni lazima tujenge taifa linalowajibika, viongozi wanaowajibika na wanaowajibishwa haraka iwezekanavyo pindi wanapofanya makosa.

Linalotia wasiwasi zaidi ni kwamba serikali haijui wanyama hai wako nchi gani kwa sasa. Ni ukweli usiofichika kwamba nyara za taifa hili zinaporwa kwa kiasi ambacho inatia fedheha kwa taifa letu. Sasa swali la kujiuliza wizara ya mali asili na utalii tujifunze nini kutoka kwenu?Mtanzania wa kawaida tu anapokamatwa hata amewinda swala mmoja tu anakamatwa je wanyama wote zaidi ya 120 wanakamatwa alafu askari wanyama pori wasione chochote? haiwezekani.

Kutokana na uzito wa suala hili hatua za haraka zinazoweza kuchukuliwa ni kuwafungulia mashtaka watu wote waliohusika na tukio hilo wakiwemo baadhi ya viongozi kama ambavyo imeshaanza kufanyika.

Kuwafutia au kusitisha leseni kwa wafanyabiashara wanaotuhumiwa.Kuimarisha ukaguzi katika uwanja wa ndege wa KIA kwa kuweka askari wa wanyama pori muda wote. Kuwepo kituo chahuduma cha askari wanyama pori katika uwanja huo ili kuimarisha ushirikiano na askari polisi, uhamiaji na forodha kwenye vituo vyote vya kutokea nchini vya mipakani, bandarini na viwanja vya ndege.

Kuimarisha kitengo cha kitengo cha inteligensia na kikosi dhidi ya ujangili kanda ya kaskazini Arusha pamoja na kuongeza vitendea kazi,watumishi na kufanya mabadiliko kwa baadhi ya watumishi. Pia wizara inatakiwa inatakiwa kuunda kikosi kazi cha kukagua mazizi yote ya kuhifadhia wanyama pori na ndege wanaosubiri kusafirishwa yanayomilikiwa na wafanyabiashara wote 180 wenye leseni. Pia vibali vyote vya kukamata wanyama vifutiliwe mbali. Mwisho kabisa wizara ifanye jitihada za kuwarudisha wanyama hai hao nchini bila kujali kama bado watakuwa hai au wamekufa.
(Chanzo: Bunge la tarehe 17/08/2011).
Posted by;
Lina James-YET 2011

No comments:

Post a Comment